Tuesday, March 19, 2013

JK asisitiza kuendelea kukopa




Rais Kikwete 
Na Waandishi , Mwananchi 

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo, kwani haiwezi kuendesha taifa kwa kutegemea kodi pekee.

Akiwa kwenye ziara ya Mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo uzinduzi wa maabara ya kisasa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Veta Kipawa.


Alisema mikopo inalipwa kwa kipindi kirefu na riba yake ni nafuu na kwamba, anashangazwa na wanasiasa ambao alidai wengi ni wasomi ambao wamekuwa wakidanganya watu na kuwatia hofu.


“Kumekuwa na siasa nyingi kwamba tunadaiwa na kila Mtanzania anatakiwa alipe Sh400,000, mnadhani tunakopa na kulipa kesho?” alihoji Rais Kikwete.
Akitoa mfano, alisema daraja la Malagarasi limejengwa kwa mkopo na kwamba, riba yake ni asilimia 0.02 na utalipwa kwa miaka 40.


“Hatuachi kukopa ng’o, ukiacha wengine kama Kenya watakwenda watachukua na kupata maendeleo halafu wewe unabaki hapohapo ulipo,” alisema.


Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewaagiza watendaji wa Dar es Salaam kujenga hospitali maalumu za uzazi na watoto, lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Alisema haiwezekani kila mara kutoa taarifa bila kuwapo kwa suluhisho la matatizo yanayotolewa ufafanuzi.


Rais Kikwete alisema katika kuboresha sekta ya afya na upatikanaji wa huduma, lazima kuhakikisha zinajengwa hospitali maalumu za uzazi na watoto ili kupunguza msongamano uliopo hivi sasa.
“Huwa najiuliza ninyi madiwani mnapokutana katika vikao vyenu mnazungumza kitu gani, kugawa viwanja?” alihoji Rais Kikwete huku watendaji mbalimbali wakiangua vicheko.


Alisema asilimia 10 ya idadi ya watu na makazi ya Watanzania zaidi milioni 44.5 wanaishi Dar es Salaam. Hivyo kunahitajika mbinu mahususi kuhakikisha upatikanaji huduma za afya.


Hata hivyo, Rais Kikwete alikataa taarifa za Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty ya kujenga Hospitali Mwambwepande akidai ni mbali, inatakiwa hospitali kuwa karibu na wananchi.


“Hiyo itahudumia watu wa Bunju na Mbweni, haiwezekani mtu wa Kimara akaenda Mabwepande hospitali zinatakiwa kuwa karibu na makazi ya watu,” alisema. Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki akitoa taarifa ya mkoa huo, alisema vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 116 kwa watoto 1,000 wanaozaliwa na kufikia 94. Pia, Rais Kikwete pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya tatu ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), jengo litakalokamilika mwaka huu.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MOI, Balozi Mstaafu Charles Mtalemwa alisema ujenzi huo utagharimu Sh17.92 bilioni zilizokopwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).


Balozi Mtalemwa alisema ujenzi utakapokamilika zitahitajika Sh8.1 bilioni, kwa ajili ya kununuliwa vifaatiba huku Rais Kikwete akiahidi kushirikiana nao kuhakikisha zinapatikana.


Wakati huohuo, akiwa TFDA Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Hiiti Sillo alisema ukosefu wa mafundi wa vifaa vya maabara, husababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa kukosa wataalamu wazalendo.


Hatua hiyo inatokana na mamlaka hiyo kulazimika kuwatafuta nje ya nchi, hivyo kuisababisha hasara Serikali ambayo hutumia zaidi ya Dola 25,000 za Marekani kila mwaka.


Rais Kikwete licha ya kusifia mamlaka hiyo kwa kutambuliwa kimataifa katika kulinda afya ya mlaji, aliwataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na ueledi ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.


No comments:

widgets

SPORTS NEWS