Tuesday, February 26, 2013

CHADEMA: Kawambwa amebakiza siku kumi

 

KAULI ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale pale na sasa amebakiza siku kumi. Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri Kawambwa jana kwamba hawezi kujiuzulu.

Akizungumza na gazeti hili(Tanzania Daima) jana, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano bado ipo pale pale.
  Alisema majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao ya kidato cha nne.

“CHADEMA tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike, ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika. Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.


Mnyika aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao kwa ajili ya elimu, zimeteketea.


Mh. Zitto Kabwe
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Kawambwa na Naibu wake, Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo. Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika. Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.


Zitto alisema kuwa rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani, na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.

Chanzo: Tanzania Daima

SWALI: NAMBA ZA SIMU ZA DR.KAWAMBWA NA AMIM AUGUSTINO ZITATOLEWA KWA WANANCHI?

No comments:

widgets

SPORTS NEWS