Friday, February 22, 2013

Wanafunzi wajiua kwa matokeo kidato cha IV


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta

Matokeo mabaya ya mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne wa mwaka 2012 yamesababisha maafa baada ya wahitimu wawili waliofeli kujinyonga.
Wahitimu waliojinyonga katika matukio mawili tofauti ni wa mikoa ya Tabora na Dar es Salaam.

Katika tukio la kwanza, mhitimu katika Shule ya Sekondari ya Kanyenye mjini Tabora ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mwinyi Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, Michael Fidelis (19), amejinyonga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, alisema mwanafuzi huyo alikwenda kuangalia matokeo Jumatatu saa 11:00 jioni huu na baadaye alikutwa amejinyonga hadi kufa chumbani kwake kwa kutumia kamba ya manila.
Kamanda Rutta alieleza kuwa marehemu alipata daraja la sifuri na kwamba aliacha ujumbe uliosomeka: “Nisamehe sana mama usitafute mchawi, nakupenda sana, uamuzi niliouchukua ni sababu ya matokeo mabaya, nakutakia maisha mema.”

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kenyenye, Kapufi Patson, alisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ni mpole na mtaratibu na wameshangazwa na uamuzi aliouchukua wa kujinyonga.
Matokeo ya shule hiyo yanaonyesha hakuna mwanafuzi aliyepata daraja la kwanza wala la pili isipokuwa waliopata daraja la tatu ni wawili, la nne ni 14 na waliopata sifuri ni 85. Wahitimu 36 matokeo yao yameuiliwa kwa sababu ya kudaiwa ada ya mtihani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo


ALIYEJINYONGA DAR
Katika tukio la pili, mhitimu katika Shule ya Sekondari Debrabant iliyopo Mbagala, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Barnabas Venant (18), amejinyonga kutokana na matokeo mabaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema jana kuwa kijana huyo, mkazi wa Nzasa, alikutwa amejinyonga kwa kamba aina ya manila ndani ya stoo ya nyumba yao.

Kamanda Kiondo alisema, tukio hilo lilitokea juzi saa 10:00 jioni baada ya kijana huyo kutoridhishwa na matokeo ya mtihani huo ambayo alipata daraja la nne, tofauti na matarajio yake.
Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.

HAKIELIMU YAKOSOA


Wakati huo huo, serikali imelaumiwa kuwa ndiyo chanzo cha matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana, kutokana na kutotumia tafiti na mapendekezo mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na asasi mbalimbali na wataalamu.

Aidha, imepewa angalizo kuwa wanafunzi watakachaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wawe ni wale waliofaulu bila ya kutumia kigezo cha kuchagua hata wanafunzi waliopata daraja la nne kwa nia ya kujaza nafasi za kidato cha tano kama ilivyofanya kwa waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Elizabeth Missokia, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu kupitia tamko kwa vyombo vya habari kuhusiana na matokeo ya kidato cha nne.

Missokia alisema HakiElimu walianza kuitahadharisha serikali na jamii kuhusiana na hali mbaya tangu mwaka 2010, baada ya asilimia 49 ya wanafunzi waliofanya mtihani kidato cha nne kupata daraja sifuri.

“Tulitoa angalizo kuwa kama juhudi za makusudi kuboresha ufundishaji na ujifunzaji hazitafanyika, basi tutarajie idadi kubwa ya wanafunzi kufeli miaka ijayo na ndicho kimetokea kwani tumeanza kuvuna tulichopanda,” alisema.

Missokia aliwaasa wananchi kuhakikisha kwamba serikali haiendelei kubahatisha katika suala la utoaji wa elimu kwa kuwa wana wajibu wa kuishinikiza kwenye suala la utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania kwa mustakabali wa taifa.

Akizungumzia watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, Missokia alisema kwa kuangalia matokeo ni dhahiri kwamba wanafunzi takribani 23,520 kati ya 367,750 waliofanya mtihani, ndiyo wanaostahili kujiunga na kidato hicho.

Alisema wanafunzi hao 23,520 wamepata kati ya daraja la kwanza na la tatu ambayo ni asilimia sita tu ya waliofanya mtihani.

“Serikali isirudie kuchukua hata wale ambao hawakufaulu kama ilivyokuwa kwa waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, ilipoamua kuchukua wanafunzi wenye alama chini ya 100 kati ya 250, uamuzi ulioonyesha dhahiri kukosa msimamo,” alisema.

Aliitaka serikali kutambua kuwa viwango vya udhahili kwa ngazi yoyote ile ya elimu hasa ufaulu, vina mantiki ya pekee kumuwezesha mwanafunzi kumudu masomo katika ngazi anayodahiliwa.

Alisema kitendo cha kuendelea kudahili wanafunzi ambao hawana sifa ni kuendelea kupeleka wanafunzi ngazi za juu za elimu, wakati hawana uwezo wa kuyamudu masomo katika ngazi hiyo.

Pia alisema HakiElimu imeshangazwa na sababu zilizotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kuwa ukosefu wa walimu na maabara ulichangia wanafunzi wengi kufeli.

Missokia alisema kuwa kati ya mwaka 2006 hadi 2009, ikama ya walimu sekondari ilikuwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 50 hadi 55, na kwamba ikama ya sasa ni ya mwalimu mmoja kwa wanafunzi kati ya 35-38, hali inayoonyesha kuvuka kiwango kinachotakiwa cha mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.

“Pia shule nyingi hazikuwa na maabara wakati huo kuliko sasa, lakini wanafunzi waliofeli sasa wamezidi kuongezeka na kufikia asilimia takribani 61. Kwa hiyo hali hii haihitaji majibu au sababu nyepesi alizozitaja waziri,” alisema.

Alitaka kuwapo mjadala wa kina kwa wananchi na wabunge kuishikiza serikali kutambua kuwa mfumo wetu hauko sawa na kubainisha changamoto za kuurekebisha haraka kupunguza athari zitakazolikumba taifa hili na mustakabali wa elimu.




CHANZO: NIPASHE

No comments:

widgets

SPORTS NEWS