Zanzibar: Imamu wa msikiti auwawa kikatili!
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi - Zanzibar
Mzee
mmoja mkazi wa Kitopeni mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar Bw. Ali
Khamis Ali (65), ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni
na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja, ACP Ahmada Khamis, alisema
kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 8.00 mchana huko kwenye
eneo la Kitope mashambani.
Alisema Marehemu Mzee Ali ambaye pia ni Imamu wa Msikiti wa Kitope mkoani hapo, alikuwa amekwenda shambani kwake kukagua mazao yake ikiwemo minazi.
Amesema alipofika shani hapo aliwaona vijana waliokuwa wakiangua nazi na
wengine wakiwa chini ya mnazi wakiziandaa ili kuondokanazo kwa maana ya
kuziiba.
Kamanda Ahmada amesema baada ya Marehemu kuwabaini wezi hao, inaonekana
kuwa alianza kupandana nao lakini walimzidi nguvu na kumchona na kitu
hicho chenye ncha kali ambacho kinaaminika kuwa ni kisu.
Amesema eneo la tukio walikuta rungu na ala la kisu ninachoaminika
kumuulia marehemu. Amesema eneo la tukio hilo pia kulikuwa na damu
nyingi na lilikuwa limevurugwa kutokana na mapambano.
Kamanda alisema baadhi ya wananchi wameitambua rungu hiyo kuwa ilikuwa
ya marehemu aliyokuwa akiitumia kwa kulindia mazao yake ambayo mara kwa
mara yamekuwa yakiibwa na wezi.
Kamanda Ahmada amesema kuwa pamoja na marehemu huyo kuuawa lakini
inaonekana pia mmoja wa wezi hao wa mazao naye amejeruhiwa katika
mapambano hayo kwani kulionekana michirizi na matone ya damu ya mtu
aliyeondoka eneo la tukio na kutokomea kusikojulikana.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo umeanza na amewataka wananchi kutoa
taarifa Polisi endapo watawaona watu ama mtu mwenye majeraha ili
akamatwe kwa kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Ahmada alisema kuwa mauaji hayo ni ya kuwania mali na
ametaka kutohusishwa na hisia za imani yoyote ama za kisiasa,
kishirikina, wivu wa kimapenzi, kulipiza kisasi ama imani za kidini.
“Haya ni mauaji ya kawaida na hayana hisia zozote. Ni mauaji kama
mauaji mengine yanayotokea katika maeneo mengine ya nchi yetu.” Alisema
Kamanda Ahmada na kuwaonya wananchi kutoweka hisia tofauti na tukio
lenyewe.
Amewaomba pia Waandishi wa Habari kutoweka maoni yao binafsi
wanaporipoti taarifa za tukio hilo ili kuepuka kuwatia hofu wananchi.
No comments:
Post a Comment